SCENE 1: -
(Ni jioni tulivu sana,upepo
mwanana toka bahari ya hindi unapuliza kwa mbali na hali kwa ujumla inaonekana
nzuri,kundi la watu limekusanyika sehemu moja na kwa ajili ya kusherekea jambo fulani .Mbele ya watu hao
yaani jukwaani amesimama Mr.Bembele mfanyabiashara mkubwa na tajiri mkubwa
jijini hapo,uso wake unaonekana una furaha sana na pembeni yake amesimama mtoto
wake wa pekee wa kiume aitwae Raymond,Kijana Raymond ni kijana mtanashati ,
mrefu na rangi yake ni maji ya kunde ametoka kuhitimu elimu yake ya chuo kikuu nchini
India,na mkusanyiko ule wa watu ulikuwa ni kwa ajili ya kumpongeza kwa hatua
ile nzuri aliyoipiga )
Mr. Bembele :( anakohoa
kidogo) Jamani habarini za jioni mabibi na mabwana…
Watu :(
wanaitikia)
Mr.Bembele: leo ni siku ya furaha sana kwangu ,na ninawashukuru wote
mlioungana nami pamoja na mwanangu wa pekee Raymond katika siku hii (ananyamaza
kidogo)mbali na mwanangu aliyefanikisha sherehe na mipango yote ni mke wangu
mpendwa Mrs.Gloria Bembele(kwa mkewe) tafadhali pita mbele uwasalimie wageni
wote waalikwa waliofika hapa kuungana nasi leo katika siku hii muhimu ya
kumpongeza mtoto wetu wa pekee aliyetupa heshima kwa kufanikiwa kuhitimu shahada
yake ya udaktari nchini India,tafadhali mke wangu pita mbele
Mrs.Bembele :(
akiwa mwenye furaha na tabasamu zuri likiwa limetanda usoni mwake anapita mbele
huku akiwa anawapungia watu mikono, baada ya hatua chache anafika alipo mumewe
pamoja na mtoto wake anachukua kipaza sauti kutoka kwa mumewe) nashukuru.
Sana kwa nafasi hii, sio siri Nina furaha sana yaani hata sijui nielezee vipi
furaha hii...
Watu :(
wanacheka)
Mrs.Bembele :(
huku anamuangalia mwanae) baba yangu mzazi maana nilikupa jina la baba
yangu...hongera sana mwanangu Mungu akulinde na kuendelea kukuheshimisha siku
zote za maisha yako…baba hongera kwa kuwa daktari, nakusihi uwe daktari mzuri
mwenye upendo na mwenye kuwajali wagonjwa maskini na matajiri, uweke utu mbele
baba kuliko pesa (anawageukia watu kisha
anatabasamu tena) nawapenda sana...na asanteni kwa kuja
Watu :( Kwa
pamoja) tunakupenda pia… (Wanapiga
makofi)
Mrs.Bembele :(
Kwa mwanae tena) nakupenda Sana baba yangu…
Raymond :(
anamkumbatia) nami nakupenda Sana mama yangu…namuomba mungu aniongoze
nikayashike Yale uliyoniambia…nakupenda sana mama yangu
Mr. Bembele (anajikoholesha
kidogo) naona Mimi sina nafasi tena eti eeh maana ni mama na mtoto...Nipeni
a Mimi hayo maupendo jamani (anaguna)
Watu (wakiwemo
Raymond Na mama yake wanaangua kicheko)
Mr. Bembele: natania najua mnanipenda sana tu sisi
ni familia moja… (kwa watu) basi sawa
mke wangu ameongea mengi sana hapa na mimi sina cha kuongezea zaidi ni kwamba
nakupenda sana pia mwanangu na nina zawadi zako maana umejua kunifurahisha mwanangu...
(Anamuita meneja wake) meneja
tafadhali nilete hizo nyaraka pamoja na funguo
Watu: wow!!!
Mr. Bembele: eti wow! Nyie watu wambea jamani (anacheka)
Meneja :(
anakuja akiwa ameshikilia hivyo alivyoagizwa na mara baada ya kumfikia Mr.
Bembele anamkabidhi)
Mr. Bembele: basi sawa mpendwa (anavipokea vitu vile) Asante tafadhali
rudi ukaketi
Meneja :(
anarudi alipokuwa ameketi)
Mr. Bembele:(kwa
Raymond) kwanza kabisa mwanangu nakupongeza kwa kuwa mtoto mwenye nidhamu
kwa watu baki na hata sisi wazazi wako, pia baba ninakupongeza kwa kuhitimu
vyema elimu yako na hatimae umekuwa daktari, (anatulia kidogo huku anamuangalia mwanae usoni) kitu cha kwanza
mwanangu nakupa kazi…kwenye hospitali yangu mwenyewe, wewe si unajua ile ni
hospitali yangu na si yako? Inakupasa sasa utafute na wewe hospitali yako…nakufungulia
kwa kukupa kazi sasa akili kichwani mwako
Raymond :(
anatabasamu) Asante baba
Mr. Bembele: utakuwa ndo boss pale…
Watu :(
wanapiga makofi) wow…
Raymond: Asante dad...Asante Sana
Mr. Bembele: sambamba na kazi hiyo nzuri lazima
boss aishi nyumba nzuri…kwahiyo nakupa nyumba mpya yenye kila kitu ndani…kama
zawadi na ina jina lako na hakuna mtu atakae kusumbua hata hapo baadae (anamkabidhi bahasha iliyokuwa na hati ya
nyumba) hii nyumba ni yako sasa ni zawadi yetu kwako
Raymond: Oh My God!!Dad…this is too much…Asante
dad…really nakushukuru Sana my dear dad…
(Anaipokea)
Mr. Bembele :(
anacheka) bado kuna zawadi nyingine…ningependa kukuzawadia…unajua ukiwa
boss bwana ni lazima utumie vitu vizuri otherwise watu watajuaje kuwa wewe ni
boss? Nakuzawadia gari Kwa ajili ya kazi zako na matembezi pia
Raymond: Oh...No Dad vitu vingine si ungeacha tu
dad…this is too much... (Anataka kulia)
Watu: aaaaawh!!!
Mr. Bembele: (anacheka
kidogo) no…usilie mtoto wangu…bado Nina zawadi yako nyingine tena najua hii
utaipenda kuliko zote
Raymond: nyingine dad?
Mr. Bembele: ndio dear leo ni mwendo wa zawadi (anageukia kwa watu kisha anamiita binti
mmoja) Christina…tafadhali njoo mbele hapa, kuna jambo nataka kuzungumza
leo mbele za watu
Christina :(
msichana Mrembo kwa muonekano wake harakaharaka ni mwanadada mwenye Maisha ya
hali ya juu. anaenda mbele Kama alivyoelekezwa, na baada ya hatua Kadhaa anamfikia
Mr. Bembele aliyekuwa amesimama mbele yeye na familia yake)
Mr. Bembele: Christina mama...
Christina: (Kwa
heshima Sana) abee baba yangu
Mr. Bembele:(kwa
watu) jamani mabibi na mabwana Christina na Raymond ni wapenzi wa muda Mrefu
sana sasa hivi wanaweza wakawa wamefikisha miaka hata kumi kwenye mahusiano yao
au nadanganya (anawageukia Raymond na
Christina)
Raymond: Ni sita tu dad… (Anacheka kidogo)
Mr. Bembele: hiyo baba sio michache… (Anawaangalia watu) nawatangazia kuwa
baada ya miezi miwili Christina na Raymond watafunga ndoa…na gharama zote za
ndoa na kila kitu nitagharamia mimi
(anatabasamu)
Watu :(
wanashangilia na waliopiga vigelegele nao walikuwepo)
Raymond :(
anaonekana hana raha na ile habari kwani ghafla tu uso wake uliokuwa na
tabasamu unazima, na tabasamu linapotea)
lakini dad…
Mr. Bembele: hakuna cha lakini hapa ushakuwa mkubwa
Raymond ni muda muafaka sasa unatakiwa kuoa na kila kitu nitagharamikia mimi… (Anawageukia watu)
Mrs.Bembele :(
anamsogeza Raymond pembeni) nini tatizo mpendwa wangu? Nakuona umekosa raha
ghafla kuna shida gani baba?
Raymond: hamna kitu mama nipo sawa (analazimisha tabasamu)
Mrs.Bembele: unanificha hata Mimi mama yako Raymond
mtoto wangu
Raymond: hapana mama kweli...Hakuna kinachonisumbua,
labda nimechoka
Mr. Bembele :(
Kwa mke na mtoto wake) kuna nini mbona sisi tunasherekea nyie
mnanong’onezana?
Raymond: tusamehe baba…
Mr. Bembele :(
anacheka) nambie Raymond baba umeipenda zawadi gani kati ya hizi
nilizokupa?
Raymond :(
bado anaonekana hana furaha) zote nzuri dad…Asante sana baba yangu
nakuahidi nitakuwa daktari mzuri na kama mama alivyoniambia nitahakikisha kila
mtu anapata huduma nzuri awe mkubwa au mdogo, tajiri au fukara wote kwangu
watakuwa sawa…Mungu anisaidie
Watu :(
wanapiga makofi)
Christina :(
anamtabasamia Raymond)
Raymond :(
anatabasamu pia lakini si kwa furaha)
Mr. Bembele
:( ananyanyua glasi) to my son…cheers
Watu :(
wananyanyua glasi pia) cheers!!!
(Muziki
unawashwa na kila mtua anaonekana ana furaha, watu wanaselebuka, wanakunywa na
kula watakavyo, sherehe imefana kweli na hakuna hata mmoja anaeonekana hana
raha isipokuwa mwenye sherehe, wakati watu wanaendelea kufurahia mama Raymond,
anagundua mwanae hana raha anamfuata)
Mrs.Bembele :(
anamfikia) hauko kawaida tangu baba yako alipotangaza kuwa unatakiwa
kufunga ndoa…baba ni nini tatizo mwanangu jamani tafadhali niambie mimi na wewe
mbona hatufichani kitu?
Raymond :(
kimya kidogo huku ameangalia chini kisha anamuangalia mama yake) mama…
Mrs.Bembele: abee mwanangu
Raymond: kwanini dad hakuniuliza Kama nataka kuoa
sasa au lah?
Mrs.Bembele: mwanangu, baba yako amefanya tu ku
assume kwamba pengine utafurahi sana akitangaza kuwa wewe na mpenzi wako wa
miaka mingi mtafunga ndoa, yeye kwake hiyo imekuwa tu kama zawadi na si
vinginevyo tafadhali usigombane na baba yako muache tu na fanya asemalo
maana…yeye ndo baba yako sa unadhani utafanyaje, (anacheka kidogo) yaani wewe mimi nikajua sijui umefanya nini
kumbe kisa hujaambiwa kuwa leo ndoa yako itakuwa inatangazwa…. mtoto una madeko
wewe loh (anamfinya sikio)
Raymond :( anacheka)
mama unaniumiza bwana
Mrs.Bembele: muone macho yake (anacheka)
Raymond :(
anatabasamu)
Mrs.Bembele: usikasirike bwana haya mambo madogo Sana…hili
sio tatizo kabisa au hutaki kuoa?
Raymond: sio hivyo mama
Mrs.Bembele: sasa baba hilo sio tatizo kabisa
mwanangu
Raymond: najua (anakaa kimya kidogo) hilo sio
tatizo mama, tatizo ni kwamba…
Christina :( anakuja
ghafla) Raymond honey… (Anambusu
mdomoni)
Raymond :(
Kwa ukali) kuwa na adabu we huoni mama yupo hapa?
Christina: mambo ya kizungu baby jamani wewe si umekaa
uzunguni…?
Raymond :(
anamkatisha) sikuwa uzunguni nilikuwa uhindini…na nimejifunza heshima
Mrs.Bembele: ongeeni taratibu tupo kwenye kadamnasi
ya watu, watu ni wengi sana acheni balaa nyie watoto, Christina nenda nyumbani
maana umelewa sana, Raymond nenda kwa watu huko hii sherehe ni yako
Christina :(
huku anaondoka) aaah!!!Wazee wengine bwana
Raymond: we Christina unasema?
Christina: naenda nyumbani
Raymond: yaani huyu mwanamke… (Anatikisa kichwa kisha anaenda walipo watu wengine)
Mrs.Bembele:sasa nimeelewa kwanini Raymond
alichukia mara baada ya kutangazwa kuwa
anatakiwa afunge ndoa na mpenzi wake kumbe wana shida kati yao hawaendani na
pia hawaelewani yaani ni kama mzungu na mchina wakiwekwa sehemu moja ni lazima
hawatafurahia uwepo wa kila mmoja wao hapo…Christina na Raymond ni wapenzi wa
miaka mingi lakini hawaelewani sasa watakuwaje wanandoa kwa hali hii?maskini
mwanangu amejiingiza sehemu ambayo yeye mwenyewe hajui atatoka vipi(anatikisa kichwa kisha anaelekea walipo
wengine)
Mr. Bembele :(
anamjia mkewe) oh my wife…ulikuwa wapi embu tufurahie mtoto wetu kamaliza
masomo yake na kesho au kesho kutwa anaanza kazi na baada ya miezi miwili
atafunga ndoa… (Anakunywa kinywaji chake)
Mrs.Bembele:ni kweli mume wangu embu tufurahie (anaendelea kufurahia sherehe ile)
1 Comments
Hello my people don't forget to visit this blog everyday for more and more stories
ReplyDelete