MUNGU MKUU 4

 


SCENE 4: -

(Mchana mtulivu, jua kwa mbali linawaka na kila mtu katika nyumba ya bwana Kenneth anaonekana anafanya kazi Fulani, wakati huo watoto yaani Ariana na Miriam wapo sebuleni, Ariana anaangalia runinga huku kwakuwa ni mdogo Miriam amelala kwenye kitanda chake cha kitoto na wakati huo anajigeuza geuzana kucheza mwenyewe huku dada yake anaonekana hana hata wazo la kumuangalia na kucheza nae)

Ariana :( anajisemea moyoni) yaani hili litoto sijui limetoka wapi yaani linaniudhi maana mama kila saa anamuangalia na kumpenda yeye…yaani amekuja kunichukulia mapenzi yote ya mama yangu

Miriam :( anaanza kulialia)

Ariana: atakoma… (Anaendelea kuangalia runinga)

Keddy :( anaingia akitokea nje) Ariana mtoto Analia humsikii?

Ariana :( anampuuzia mama yake)

Keddy: nakuongelesha, kwanini mdogo wako Analia humbebi?

Ariana: huyo sio mdogo wangu mama, sio mdogo wangu kabisa, huyu si mlimkuta hapo nje, simjui…sio damu yangu

Keddy :( anajishusha) mwanangu, pamoja na hayo, huyu mtoto tumemchukua na kumfanya mtoto wetu hauna budi kumkubali

Ariana: kwani mama huwezi kunipa mdogo wangu wa kiukweli ukweli?

Keddy: Mungu mkuu mwanangu amenipa mtoto kwa njia yake anayoijua mwenyewe, mwanangu…

Ariana: hapana mama…nakwambia kabisa kuwa sitaweza kumkubali huyu mtoto Kama mdogo wangu hata siku moja…kwangu Mimi atabaki kuwa mtoto wa nje na sio mdogo wangu…

Keddy: nikuambieje mwanangu ili uelewe

Ariana: siwezi kuelewa hata kidogo na nafsi yangu imekataa kumkubali Miriam kama mdogo wangu

Keddy: sawa sina usemi (anamnyanyua Miriamna kuingia nae ndani)

Ariana: Hilo litoto ndo sababu ya mimi kukosa mapenzi yako mama

Keddy :( anarudi) mwanangu tulikaa miaka kumi na mbili bila kupata mtoto mwingine…wewe mara zote mwanangu ulililia mdogo wako na kila mara nilishindwa kukupa mdogo wako mwanangu kwasababu ya kwamba daktari aliniambia sina uwezo wa kushika tena mimba

Ariana: mama wewe sio mgumba ungesubiri tu Mungu angekupa tu mtoto mama na sio kuniletea mtoto sijui ametoka wapi na mbaya Zaidi unampenda Zaidi yangu

Keddy: huo sio ukweli mwanangu nawapenda wote Zaidi na Zaidi wote ni wanangu na ninawapenda sana wanangu…na hata Mungu analijua hilo

Ariana: mama unampenda sana huyo mtoto ambae hatujui ni mtoto wa nani kuliko mimi mwanao wa kumzaa kila saa ni yeye tu, mimi hata hujui nina tatizo gani wewe unawaza tu kuhusu huyu mtoto

Keddy: hiyo sio kweli mwanangu mbona hata wewe nakupenda mama

Ariana :( machozi yanamlenga) natoka shuleni hata hujui Kama nimerudi au sijarudi wewe kutwa nzima kumuangalia huyo mtoto

Keddy: lakini huyu bado mdogo na anahitaji kuwa na uangalizi mkubwa…

Ariana: yupo ma mdogo Mary yupo na mpaka huwa anamnyonyesha inamaana anaweza kumuangalia vizuri kwanini mama huna muda na mimi na ndo mwanao wa kumzaa...

Keddy: huelewi mwanangu…hata kama ningezaa mtoto ni lazima ningekuwa ninamuangalia Zaidi yako

Ariana: ingekuwa bora maana ningejua kuwa ni mdogo wangu wa tumbo moja wala ninsingekuwa nina shida na hilo ila huyu mama sio mdogo wangu mama…

Keddy: lakini ni zawadi na kwa kawaida ya zawadi ni kuipokea na kuitunza mwanangu

(Wakati huo Mary ambae pia ndo mama wa mtoto Mirriam amesimama pembeni yao na anawasikiliza yote wanaozungumza)

Keddy: nikuambiaje Ariana ili uelewe kuwa Miriam hayupo hapa kukuchukulia nafasi yako, nafasi yako itabaki kuwa yako

Ariana: hatuwezi kufika mwisho mama bora tu uniache mama…na sitawahi kumkubali huyu mtoto kama mdogo wangu atabaki kuwa mtoto mliomuokota…

Keddy: nitakupiga sasa, usisahau kuwa mimi ni mama yako na ni lazima uongee na mimi kwa adabu usione kuwa nimenyamaza ukaona sina akili…nakuvumilia kwakuwa nakupenda na kumbuka ni wewe ndo ulikuwa unataka mtoto sasa nimeshangaa Mungu katupa zawadi unaleta ujinga kuwa makini Ariana

Ariana: nakubali kuwa nilitaka mdogo wangu…nimepata ila siwezi kumkubali maana sio ndugu yangu

Keddy: undugu sio kufanana, ni kufaana mwanangu sasa mimi nitatoa wapi mtoto huku nimekwambia sina uwezo tena wa kupata mtoto…mkubali tu huyu mtoto na utakuwa tu na Amani mwanangu jitahidi kumchukulia tu kama mdogo wako na utaona kuwa maisha sio magumu

Ariana: No! Siwezi kumchukulia kama mdogo wangu

Keddy :( anaondoka huku amembeba Miriam) ngoja nimlaze mtoto maana ubishi wako mpaka mtoto amelala

Ariana :( anaonyesha kukasirika)

Keddy :( anamlaza mtoto)

Ariana: kila kitu imekuwa yeye yaani mpaka mimi naonekana sio mtoto wa hapa bali yeye

Mary :( anakuja alipo Ariana) Ariana mwanangu

Ariana :( anamkatisha) najua na wewe upo hapa kumtetea huyo mtoto hakuna anayenipenda hapa…kila mtu ananichukia na kuniona sifai

Mary: hiyo sio kweli Ariana mwanangu…Mimi mbona nakupenda sana

Ariana :( huku anaondoka) huo ni uongo mtupu (anabamiza mlango wake kwa hasira)

Keddy :( anatoka chumbani kwake kwa haraka) nini hicho?

Mary: Ariana amebamiza mlango…anaona kila mtu hampendi kisa Miriam…

Keddy: muache tu…atageuza mawazo kikubwa tuendelee kumvumilia

Mary: unampenda kweli Miriam, dada yangu utasema ni mwanao wa kumzaa

Keddy: ni zawadi toka kwa Mungu nahisi Mungu alinisikia kilio changu cha muda mrefu nahisi nilikuambia kuhusu stori yangu ya kutopata mtoto kwa muda mrefu mara baada ya kumzaa mwanangu Ariana…kama nilivyokuambia mwanangu Miriam nilimkuta hapo nje…mama yake alimuacha hapo nje

Mary: mmeshawahi kumtafuta mama Mirriam?

Keddy: hapana na wala sitaki kumjua maana atamchukua mwanangu

Mary: na siku mama yake akitokeza je?

Keddy: sitaki hata kujua na kufikiria kitakachotokea mara baada ya mama yake Miriam kutokea ila nitamuomba tu asinichukulie zawadi niliyopewa na Mungu

Mary:(anajisemea moyoni) mama yake Miriam ni mimi dada, na wala sitamchukua hata siku moja maana unamlea kama mwanao wa kumzaa upo tayari kugombana na mwanao kisa mwanangu kweli unampenda mwanagu kama mwanao wa kumzaa, kwanini nimchukue hii siri itabaki moyoni mwangu milele na milele(anatabasamu)maskini anaona ni zawadi kutoka kwa Mungu kweli huyu mwanamke ni mtu mzuri sana…sasa sijui mwanae kamchukua nani maana hata hawaendani tabia

Keddy: unaonekana kuna kitu unawaza, unawaza nini…mwenzangu?

Mary :( anacheka kidogo) wala sina chochote nachowaza…

Keddy: tupike shoga yangu shemeji yako anakuja sasa hivi kula kwahiyo tumalize kupika haraka

Mary: nishapika mbona mie…

Keddy: uko vizuri mwaya

Mary :( anatabasamu) Asante mwaya

Keddy: je unadhani kuwa ipo siku Ariana atamkubali                          

Mary: atamkubali tu…endelea kumbembeleza atamkubali tu ipo siku…

Keddy: tujipe moyo mwenzangu tutashinda

Mary: kabisa…ipo siku watakaa na kufurahia maisha pamoja mpaka utakuja kufurahi na kushangaa wewe wape muda tu

Keddy: na unapenda kweli kunipa moyo mwenzangu

Mary: ndo ukweli wenyewe

Keddy: Asante mwaya

Mary: haya usijali dada yangu

Keddy: haya asante kwa kunipooza shoga yangu…. naomba tukatenge huyu akija akute tayari tumeshapika na kutenga

(Kwa pamoja wanaenda kutenga chakula na wanatenga huku wanaendelea kuongea mambo tofauti tofauti na wanaonekana wanafurahia na maana wanacheka)

Post a Comment

0 Comments