MUNGU MKUU 3

 


SCENE 3: -

(Asubuhi ya siku nyingine Mary yupo jikoni akiwaandalia watoto na wenye nyumba chai na kumuandaa Ariana kwa ajili ya shule)

Keddy :( anakuja akiwa amembeba mtoto Miriam) za asubuhi Mary…

Mary: salama dada shikamoo…

Keddy: marahaba…umeamkaje?

Mary: salama tu…

Keddy :( anamuangalia mtoto) yaani ana njaa kweli huyu, fanya mpango wa maziwa nadhani yapo kwenye friji fanya hivyo mdogo wangu

Mary :( anajikuta anaropoka ghafla) mlete nimnyonyeshe…

Keddy: (anashangaa) umnyonyeshe? (Anacheka kidogo) utamnyonyeshaje?

Mary :( anajichekesha) unajua…dada…Mimi mwenyewe nimetoka kujifungua yaani sina hata wiki…

Keddy: mtoto yuko wapi?

Mary :( anasikitika kidogo) amefariki…

Keddy: Oh…maskini pole Sana…najua inavyouma kwa mama kumpoteza mtoto wake…Mungu atakutetea usijali mdogo wangu

Mary: Asante dada… (Anamchukua mtoto) maskini kaone kanavyotetemeka...

Keddy: njaa mbaya…tangu amekuja tunamnywesha maziwa ya ng’ombe maana Mimi sio mama yake nadhani nilikuambia ila nitamlea Kama mwanangu wa kumzaa kabisa

Mary: Mungu akakubariki wewe na familia yako milele na milele kwa kumtunza huyu kiumbe ambae hamjui hata ametokea wapi…

Keddy: Mimi na mume wangu tumetafuta mtoto huu ni mwaka Zaidi WA kumi, Ariana alitusumbua kuwa anataka mdogo wake mpaka tukajuta ila Mungu amejibu maombi yetu kwa kutuletea huyu mtoto…

Mary :( huku anakaa Ili amnyonyeshe mtoto) mungu ni mkuu na fadhili zake ni za milele na pia njia zake hazichunguziki kabisa…

Keddy: hakika…

Ariana :( anakuja akiwa anatokea chumbani kwake) shikamoo mama…

Keddy: marahaba mwanangu umeamkaje mama?

Ariana: salama… (Anamuangalia Mary) shikamoo…anti

Mary: marahaba…

Ariana: iiii, mama mbona anamnyonyesha mtoto?

Mary :( anacheka kidogo) Mimi mwenyewe nimetoka kujifungua juzi juzi tu ila mwanangu amefariki

Keddy: usiogope…mwanangu…Miriam ni mdogo wako tu (Anatabasamu huku anamshika nywele zake)

Ariana: Mimi nataka tu mdogo wangu wa tumbo moja…mama kwani haiwezekani?

Keddy :( anamuangalia)

Ariana: nataka tu mdogo wangu wa tumbo moja

Keddy: Ariana tafadhali usianze tena shida zako we mtoto

Ariana :( anavuta mdomo)

Keddy: naomba ukaoge uwahi shule…

Ariana :( anaingia chumbani kwake)

Mary :( amekaa kimya)

Keddy: yaani huyu mtoto…

Mary: Ni utoto tu dada hata usijali kabisa na kila kitu kitakuwa sawa na unaweza kushangaa akaja kumpenda kama mdogo wake wa tumbo moja kikubwa ni kumvumilia tu, mpeni muda tu dada

Keddy: sawa bwana kama unachosema kitakuwa basi Bwana akubariki

Mary :( anacheka) narudia kusema usimkatie tamaa

Ariana :( anatoka kuoga anakuja jikoni) chai iko wapi mi nataka kwenda shule

Keddy :( anatabasamu) yaani unawahi huku anayekupeleka hajaamka bado

Ariana: inamaana hunipeleki wewe?

Keddy: hapana…Mimi nabaki na mtoto

Ariana :( anashikwa na hasira sana)

Mary: usijali…Ariana…mama atakupeleka (anamgeukia keddy) dada mpeleke tu…Mimi nitabaki na kichanga nitamuangalia vizuri…

Keddy: sawa… (Anaingia chumbani kwake) mume wangu (anamgusa) amka baba…mbona leo umelala sana?

Ken :( anajigeuza) ah…uchovu tu mama…vipi Ariana ameshaenda shule?

Keddy: ndo naoga nimpeleke

Ken: Miriam atabaki na nani? Acha tu nimpeleke hata hivyo nataka kwenda kazini sasa hivi

Keddy: Ariana anataka apelekwe na mimi…

Ken: Ariana nae ana masharti kweli…haya mpeleke ngoja na mimi nijiandae niende kazini

Keddy: sawa, ngoja nioge haraka (anaingia bafuni)

(Upande wa Ariana na Mary)

Ariana: ila huyo mtoto ni wako eti ee?

Mary: (anashtuka) kwanini unasema hivyo?

Ariana: mbona unamnyonyesha Kama sio mwanao?

Mary :( kimya)

Ariana: nakuuliza…nijibu

Mary :( anajichekesha) Ariana bwana…si nimekuambia kuwa nimejifungua juzijuzi tu na bado natoka maziwa…kwanini yakae hivyohivyo huku kuna mtoto anayahitaji?

Ariana: haya bwana Kama ni hivyo

Mary: uko darasa la ngapi?

Ariana: la Saba…

Mary: kumbe unamalizia…

Ariana: ndio… (Anamalizia kunywa chai)

Mary: Ariana mpende Sana mdogo wako huwezi jua Mungu ana makusudi gani kwa kumleta huyu

Ariana: kwani Mungu ana makusudi gani?

Mary :( anakaa kimya)

Ariana: nachojua huyu sio mdogo wangu na hata siku moja sitampenda kama mdogo wangu

Keddy :( anatokea chumbani na kusikia maneno yale) Ariana…

Ariana: siwezi kujifanya kumpenda huyu mtoto…siwezi tu kufanya hivyo nisameheni Kwa kweli

Keddy: umeingiwa na nini Ariana?

Ariana: sio mdogo wangu tumbo moja…mama hata hatumjui katoka wapi na mama yake ni nani je wakiwa ni watu wabaya?

Keddy: Miriam ni malaika tu mwanangu hana hata hatia yoyote…ni zawadi ambayo Mungu ameamua kutupatia wewe huoni fahari kuwa na mdogo mzuri?

Ariana: mama nachelewa shuleni…

Mary :( anajisemea moyoni) hili ni tatizo…eeh…Mungu mnusuru mwanangu na Ariana…

Keddy: Mary…kaa na mtoto nakuja baada ya muda kidogo ngoja nimpeleke huyu shuleni

Mary: sawa dada

(Keddy na Ariana wanatoka nje na kupanda kwenye gari na mara baada ya kukaa kwenye gari, Keddy anawasha gari na bila kupoteza muda wanaondoka kuelekea shuleni huku kila mmoja wao amekaa kimya na hataki kumuongelesha mwenzie)

Keddy :( anavunja ukimya) nakupenda mwanangu

Ariana :( kimya huku anaangalia pembeni)

Keddy: (anaamua kukaa kimya)

Post a Comment

0 Comments