SCENE 59: -
SHEREHE YA HARUSI YA ANGELINA NA RAYMOND UKUMBINI:
-
(jioni tulivu,kuna manyunyu Fulani ya mvua,watu wengi sana
jamaa,ndugu,marafiki hata majirani wa Angelina na Raymond wamekusanyika katika
ukumbi mkubwa tena wa kifahari kuliko kumbi zote jijini hapo,watu
wanakunywa,wanafurahi kabla ya sherehe yenyewe kuanza,miongoni mwa matukio ni
tukio la red carpet kabla ya mambo yote,watu wanapita wakiwa wamependeza katika
zuria jekundu lililowekwa kwa ajili ya wageni wote.Nyuma ya jukwaa la mahojiano
kumebandikwa picha kubwa sana yenye sura za Angelina na mumewe na kuna maneno
yameandikwa “welcome to wedding reception of Raymond and Angelina)
Mtangazaji: wow… (anaangalia camera) karibuni mabibi na mabwana katika sherehe ya
harusi ya Angelina na Raymond, kwa kuanza kabisa naomba nipige stori mbili tatu
na wageni waalikwa kabla hawajaingia ukumbini kushuhudia yaliyo humo (anamgeukia
mgeni wa kwanza ambae ni Christina) wow…dada mambo
Christina: poa…
Mtangazaji: umependeza Sana
Christina: Asante Sana…
Mtangazaji: kwanza kabisa tuanze na kichwani nywele
tamu hiyo toka wapi?
Christina: hii nywele tamu toka nywele classic wapo
Kariakoo msimbazi mkabala na big born sheli
Mtangazaji: wow…na nani kakuvalisha?
Christina: nimevalishwa na gauni pambe pia wapo
Kariakoo…
Mtangazaji: barabara kabisa…na pochi nzuri toka
wapi?
Christina: pochi nzuri hii toka jumba la pochi nao
wapo Kariakoo
Mtangazaji: Safi na kucha nani kakutengeneza?
Christina: mwenyewe (anacheka)
Mtangazaji: na viatu…
Christina: shoes online
Mtangazaji: Safi na (anamuangalia Peter aliyekuwa amesimama pembeni ya mkewe) na kaka hapo
umependeza sana
Peter: Asante Sana…
Mtangazaji: unajisikiaje kuwa mmoja wa wageni
waalikwa leo kwenye harusi kubwa inayotikisa Dar?
Peter: najisikia vizuri na furaha pia…kuwa miongoni
mwa wageni waalikwa kwenye hafla ya kuwapongeza ndugu zetu kwa kufunga ndoa
Mtangazaji: Asante Sana...Karibuni mburudike (anaenda Kwa wazazi wa Raymond)
shikamooni
Wazazi: marahaba...
Mtangazaji: mmependeza
Wazazi: Asante Sana
Mtangazaji: mnajisikiaje kuwa katika sherehe hii?
Mr. Bembele: Nina furaha tu toka asubuhi mchana na
mpaka sasa hivi mwanangu kaoa nina furaha sana
Mtangazaji: oh, kumbe wewe ni baba wa bwana harusi?
Mr. Bembele: ndio…we huoni chata hii
Mtangazaji: nawaona…kweli mmefanana Sana
Mr. Bembele: ndo hivyo
Mtangazaji :( anacheka
kidogo) basi sawa haina shida karibuni ukumbini
Wazazi: Asante Sana (wanaingia ukumbini)
(Mtangazaji
anaendelea kuhoji watu mbalimbali ikiwemo ndugu zake Angelina na marafiki
waliokuja kuungana pamoja katika hafla ya kuwapongeza maharusi wa siku hiyo,
mahojiano yanaendelea kwa muda na hatimaye wanaisha na kila mtu akiwemo
cameraman na mtangazaji wanahamia ukumbini. Ukumbi umependeza sio mchezo na
unang’aa kweli kweli na watu wanaonekana kwa uzuri kabisa. Kila mtu anaonekana
kufurahi sana)
Mc: jamani mnafuraha nyie
(Watu wanacheka)
Mc: kwanini sasa?
Watu: Raymond kaoa…
Mc: kumbe???Sikujua naona tu shamrashamra watu
hawatulii makamera mpaka juu ya vichwa vyetu kumbe Ray ameoa? Basi sawa bila
kupoteza wakati mtakuwa nami mc wenu, mc mjanja kuliko hao wote Mc
Rugemalira…yaani Mc Ruge…pigeni basi makofi
Watu :(
wanapiga makofi)
Mc: basi sawa naomba niuruhusu msafara wa maharusi
wetu…waingie ukumbini…Dj fanya yako baba
(unapigwa
muziki mzuri na msafara wa maharusi yaani mabrighter wakike na wa kiume
wanaingia wakiwa wanacheza vizuri sana, miongoni mwa mabrighter wa kike ni
wadogo zake Angelina na wa kiume yupo mdogo wa Angelina pia, wanacheza vizuri
sana na watu wanawashangilia sana, wanacheza na mwisho wanafika mbele)
Mc: Dj tulia kidogo… (Kwa watu) jamani wamependeza hawajapendeza?
Watu: wamependezaaaaaaa
Mc :( Kwa Dj)
niletee matron Na bestman tafadhali
(Dj anaachia
muziki mzuri na Edmond pamoja na mkewe wanaingia wanacheza kwa madaha yote,
kama ilivyo kawaida ya watu wanacheza na kufurahi sana, wanashangilia sana. Edmond
wanasakata rhumba mpaka wanafika mbele wanapofika mbele wanasimama kusubiri
maharusi waingie)
Mc:(kwa Dj) kamatia hapo (kwa Edmond na mkewe)
mmependeza…
Edmond na Catherine: asante (wanatabasamu) asante sana…
Mc: basi sasa ni wakati wa kuwakaribisha bibi na
bwana harusi… (Kwa Dj) embu niletee
hao waliotufanya tukutane pamoja hapa leo
Dj :( anaachia
wimbo mzuri Sana unaoendana nao)
(Maharusi
wanaingia wakiwa wamebadili nguo tofauti na zile walizokuwa wamevaa asubuhi
wakati wa kufunga ndoa, Angelina amevaa gauni aina ya nguva lililombana vyema
na kumonyesha umbo vizuri na pia lina mkia mrefu kiatu alichovaa ni kirefu
sana,mtoto wa Kihangaza ameng’aa ukimuangalia kweli unakubali,kwa upande wa
amevaa suti aina ya taxedo ya rangi ya kijivu na kiatu cheusi
amependeza.Maharusi hao wanaingia wakiwa wanacheza kwa furaha sana na kufanya
kila mtu atambue kuwa wana furaha ya kuwa mume na mke.Baada ya kucheza kwa
madoido kwa muda kidogo hatimaye wanafika mbele,wanapokelewa na mabrighters,wanaowasindikiza
karibu kabisa na meza yao yaani High Table)
Mc:(anashusha pumzi kidogo) kwani bibi harusi wewe
kabila gani?
Angelina: mhangaza...
Mc: ndo wazuri hivyo…He!!Naoa wahangaza mie…cha
kufia nini?
(Watu ikiwemo Angelina mwenyewe wanacheka)
Mc: basi sawa…kabla hatujapoteza muda Zaidi kuna
kamchezo fulani tunaenda kucheza hapa kabla ya utambulisho na kila kitu…huo
mchezo unaitwa (anavuta viti viwili)
shoe game…nyie maharusi njooni make hapa…vueni viatu, wewe bibi harusi shika
kiatu kimoja cha mumeo na chako na wewe bwana harusi shika chako na cha mkeo
Maharusi :( wanafanya
Kama walivyoambiwa)
Mc: nyinyi mabrighter kaeni jamani muenjoi…hii ni
harusi ya masteringi…
(Watu wanacheka)
Mc :( kwa
maharusi) mko tayari kwa mchezo huu? (kwa
watu) mko tayari?
Watu: tuko tayariiiii
Mc: Safi…naanza, iko hivi nikiuliza swali Kama jibu
ni bibi harusi mnanyoosha kiatu cha bibi harusi na jibu kama ni bwana harusi
basi kiatu cha bwana harusi kinanyooshwa…haya tunaanza
Maharusi: tuanze
Mc: swali la kwanza, nani alikuwa wa kwanza
kumpenda mwenzie?
Angelina:(ananyoosha
kiatu chake)
Raymond :( ananyoosha
kiatu chake)
Mc: hakuna kuangalia nyuma (anashangaa) kwahiyo jibu ni bibi na bwana harusi… (Anaguna) kwahiyo wote mlianza kupendana
Raymond: Mimi ndo nilianza
(Watu wanacheka)
Mc: nani alianza kumwambia mwenzie hisia zake?
Maharusi :(
wananyanyua kiatu cha Raymond Kwa pamoja)
Mc: wow…swali lingine…nani kati yenu ni mbishi
jamani yaani akibisha hata dagaa haoni ndani
Maharusi :(
wananyanyua kiatu cha Angelina Kwa pamoja)
Watu :( wanacheka
Sana)
Mc: nani…mgomvi…
Maharusi :( wananyanyua
kiatu cha Raymond Kwa pamoja)
Mc: nani ndo anapenda kushika rimoti?
Maharusi :(
wananyanyua kiatu cha Angelina)
Raymond: halafu sasa anaweka ma muvi ya kihindi
halafu analala…ukitoa, akishtuka utakubali muziki…
Angelina :( anacheka
Sana)
Watu :( wanacheka
pia)
Mc :( anacheka kidogo)
nani anapenda kudeka?
Maharusi :( wananyanyua
kiatu cha Angelina)
Mc: nani ana upendo Kwa ndugu?
Maharusi :( kila
mmoja wao ananyanyua kiatu cha mwenzie)
Watu: wow...
Mc: basi naona bibi harusi kashinda kwenye mchezo
huu mfupi… (Kwa watu) mmefurahia?
Watu: saaaana endelea
Mc: ah inatosha…sasa rudini (kwa maharusi) mkakae na ratiba nyingine ziendelee
(Maharusi wanaenda kukaa)
Mc: utambulisho sasa…
(Maharusi wanatambulisha ndugu zao, jamaa na marafiki zao kwa nyakati
mbalimbali, wakitambulishwa kwa nyakati tofauti wananyanyuka na kuwapungia watu
mikono, utambulisho unaendelea na baada ya muda utambulisho unaisha)
Mc: sasa naomba wasukuma mje mtuchangamshe kidogo
maana nimeambiwa bwana harusi ni msukuma wa Mwanza naombeni mje mtupe mambo
(Wasukuma na watu mbalimbali wanapita mbele kucheza ngoma za kwao)
Mc: Asante Dj…sasa jamani zawadi…
(Watu
mbalimbali wanajiandaa Kwa zawadi)
Mc: vikundi ni vingi jamani hawa watu wanaonekana
wanaishi na watu vizuri sana…nitatoa utaratibu wa zawadi msijali wote mtapata
nafasi ya kutoa zawadi
(Watu wanajiandaa)
Mc: tunaanza na wazazi…wa pande zote mbili…
(Wazazi wa pande mbili wanapita mbele yaani Mr and Mrs Bembele pamoja na
mama mzazi wa Angelina)
Mc :( anampa
kipaza sauti baba mzazi wa Raymond)
Mr. Bembele :(
anapokea kipaza sauti hicho) harusi Safi?
Watu: safiiiii
Mr. Bembele: asanteni sana mabibi na mabwana,
nafuraha sana…nakumbuka mwaka kama mmoja uliopita nilisimama mbele ya watu kama
hivi nikampa zawadi nyingi sana kijana wangu aliyekuwa amehitimu shahada yake
ya udaktari sasa leo tena nimepewa nafasi kuwazawadia watoto wangu wawili wa
kike na kiume…
Watu :( wanashangilia
Sana)
Mr. Bembele: asante kijana wangu kwa kunipa
binti…nilikuwa nina mtoto mmoja tu ila kwa ajili ya mwanangu nimepata binti… (kwa Angelina) karibu sana binti yangu
Angelina :( anapiga
magoti) Asante baba
Mr. Bembele: Asante mwanangu
Raymond :( analengwa
machozi na anajikuta Analia kwa furaha)
Mr. Bembele: nawapenda wanangu…sisi wazazi wenu
tunawapa zawadi ya nyumba moja na mapumziko ya nchi za ulaya kwa muda wa mwezi
mmoja, kuzungukia nchi mbalimbali za ulaya ndani ya mwezi mzima (anawapa pasipoti zao)
Watu: wanashangilia Sana
Mr. Bembele :(
anawakabidhi pia hati za nyumba)
(Baada ya zawadi hiyo wazazi wa pande mbili
wanarudi kukaa, zawadi zinaendelea kuletwa kwa maharusi hao wanaopendwa sana na
watu,watu wanacheza,wanakula,wanapiga picha wanafurahia sherehe hiyo,wazazi
wana furahi,wafanyakazi wa Raymond wa ofisini na nyumbani wanaonekana wana
furaha kubwa,marafiki wa Raymond na Angelina nao wanafurahi sana,Christina
ambae alikuwa ndo kizingiti kikubwa katika penzi la Angelina na Raymond nae
anaonekana kuwa na furaha kubwa sana yeye pamoja na hawara yake wa zamani na
mume kwa sasa,mambo ni burudani,wadogo zake Angelina nao wanaonekana kufurahi
sana,picha zinapigwa za ukumbusho kwa ndugu jamaa na marafiki,kila kitu
kinaonekana kupendeza na siku hiyo inakuwa ni siku nzuri kwa Angelina,Raymond
pamoja na familia zao.Angelina ni mke halali wa aliyekuwa bosi wake Bw.Raymond Bembele
kijana tajiri na mtoto wa pekee wa mfanyabiashara tajiri jijini hapo.harusi
imefana kwelikweli na ni ya kifahari kwelikweli,watu
wamekula,wamekunywa,wamepata zawadi mbalimbali,kuna burudani kutoka kwa wasanii
mbalimbali hasa waimbaji wa nyimbo za injili,ni harusi ya kukumbukwa.)
0 Comments